Thursday, September 18, 2014

UJUMBE MUHIMU KUTOKA KWA MKUU WA MSAFARA WA WASANII BUNGENI DODOMA, SIMON MWAKIFAMBA RAIS WA TAFF

TAARIFA KWA WASANII WOTE WA TANZANIA, NAOMBA IELEWEKE MCHAKATO WA HOJA ZA WASANII KUWEPO KWENYE RASIMU YA KATIBA SI KWA MASLAHI YA TAFF AU TDFAA NI KWA MASLAHI YA WASANII WOTE WA NCHI HII.KAMA UNAONA JAMBO HILI LINA MSLAHI UNGANA NASI,KAMA UTASHINDWA KWA KUTOKUWA NA UWEZO TUTAKUWAKILISHA NA KAMA HALIKUHUSU UBARIKIWE.SAFARI YA DODOMA IPO JUMAPILI 21 SEPTEMBA.SIMON J MWAKIFWAMBA KIONGOZI WA MSAFARA KWA SANAA ZOTE

Wednesday, September 17, 2014

NYAMAYAO AJA NA JOYCE

Msanii mkongwe aliyewahi kutamba sana katika kundi la Kaole Sanaa Group, amevunja ukimya anakuja na mzigo huu, hebu muunge mkono kwa kununua nakala halisi halafu uangalie uone ukweli wa msemo "Ng'ombe Hazeeki Maini"

ACTION & CUT VIEWERS CHOICE AWARDS 27TH SEPTEMBER 2014 SUNRISE BEACH KIGAMBONI





Popote duniani kinacholeta mvuto ni kile kinachoshindaniwa, hata mpira usingekuwa na mashindano, kusingekuwa na msisimko wala wapenzi wa soka...Kwa hatua hii nadhani kila mmoja atakuwa makini, ombi langu, chonde chonde tuzo hizi ziendelee. Maana nakumbuka kwa mara ya kwanza katika historia ya kiwanda cha filamu nchini kulikuwa na tuzo za Vinara mwaka 2008 baada ya hapo kimyaa!! Zikaja tuzo za Bora wa 2010 baada ya hapo kimyaa!! Zikaja tuzo za Steps mwaka 2013 baadae zii!! Sasa zamu ya Action & Cut Viewers Choice Awards, sijui baada ya hapo kaburi limeshachimbwa? Only God knows!! Ila Big up sana kwa waandaaji.www.facebook.com/Ali Yakuti

Tuesday, May 8, 2012

FROM SCRIPT WRITER TO DIRECTOR

                                       Hapa niko na cameraman wangu aitwaye Seif Puche

      Mwaka huu wa 2012, nimeamua kuingia kivingine zaidi katika tasnia, sasa hivi nimeamua kuvaa kofia nyingine kadhaa baada ya hii ya uandishi wa script kunitosha vema. Sasa hivi ninavaa kofia ya Producer na Director, bila kusahau nitakuza zaidi nafasi yangu ya uigizaji ili kuleta changamoto katika tasnia. Kaeni mkao wa kula mzigo mpya chini ya uandishi na uongozaji wangu utaingia sokoni muda wowote. Kuwa nami niweze kukujuza mzigo huo unakwenda wa jina gani na utaupata wapi?.

                            Bi Mwenda na Irene Paul wamo katika filamu hii ya kusisimua

                Hapa niko na Irene Paul baada ya kukamua scene kwa kiwango kikubwa

                                             Kupa naye yumo katika mzigo huu, hebu pima

                       Hapa Chopa Mzee wa Halmashauri ya Kichwa akikamua na Kupa

                                                  Mpambano mkali!! Chopa na Irene Paul

Sunday, April 29, 2012

NYAKATI AMBAZO NI NADRA KUSAHAU


                               Mimi  na hayati Steven Kanumba baada ya kuchukua tuzo zetu mwaka 2010

         Kuna tatizo hili Tanzania, sijui niseme ni sugu au niliiteje? Hakuna chombo au taasisi maalumu inayohusika moja kwa moja na utoaji wa Tuzo za Filamu....Sijajua sababu hasa ni nini. Mwaka 1999, kulikuwa na Tuzo zilizojumuisha kada mbali mbali filamu ikiwa mojawapo, na ninakumbuka aliyeibuka kuwa msanii bora wa kiume alikuwa Richie Richie, wengine siwakumbuki pengine kwa sababu hawapo tena kwenye tasnia, tuzo hizo ziliandaliwa na M-net. Mwaka 2006 (Kama sikosei), kul,ikuwa na Tuzo za Risasi zilizoandaliwa na Gazeti lka Risasi, na msanii bora wa kiume alikuwa Dimoso, wakati msanii bora wa kike alikuwa Riyama. Mwaka 2008 kulikuwa na Vinara Awards ambapo Msanii bora wa kiume alikuwa Jacob Steven na Msanii bora wa Kike alikuwa (Simkumbuki jina) ila Irene Uwoya na Yusuf Mlela walipata tuzo ya up coming wakati Steven Kanumba akiambulkia tuzo ya heshima. Mwaka 2010 kulikuwa na tuzo za Filamu Central, ambapo Mimi nilishinda nafasi ya mwandishi bora wa Mwaka, Steven Kanumba alishinda Mugizaji bora wa Mwaka, Monalisa lishinda muigizaji bora wa kike wa mwaka, Vincent Kigosi alishinda tuzo ya muongozaji bora wa mwaka na mtayarishaji bora wa mwaka. Kukafuatia tuzo ambazo hazina utaratibu na hata zote ambazo nimekuwa nikizitaja huwa zinafanya mara moja halafu hazirudii tena, labda ZIFF kidogo naona wana utaratibu wa kuwa na tuzo kila mwaka, sijui sasa watu huandaa wakiwa wanatarajia kitu tofauti na uhalisia? Hebu tuchangieni

Wednesday, April 25, 2012

NYAKATI ZA KUKUMBUKWA

    Hapa nilikuwa namwelekeza kitu wakati wa upigaji picha ya                  Family Tears 2008

      “Hakuna kitu kizuri duniani kama kuifanya dunia hii kuwa darasa kwako, jifunze kwa kila mtu, hata kichaa aweza kuwa mwalimu kwako, kama hutajifunza chochote toka kwa kichaa basi hata kutoautisha tu mwenye akili kwa kumlinganisha na huyo kichaa ni darasa tosha…” 
      Nakumbuka maneno haya nilimwandikia Hayati Steven Charles Kusekwa Kanumba katika moja ya script chakwa zilizomkuza na ikawa ni dira katika maisha yake. Nitaikosa sana tabia yake hii ya kuwa msikilizaji kuliko mbishani, alipenda sana kujifunza na kudadisi mno kwa kitu ambacho hakukijua, hakuwa mjuvi kwa jambo asilojua, na akilijua basi hulizingatia, Tunapaswa kuiga tabia hii kama kweli tunataka kubakisha historia nyuma yetu.

Monday, April 23, 2012


TAMKO RASMI KUHUSU SHUTUMA DHIDI YANGU JUU YA KIFO CHA KANUMBA

Yapata wiki tatu sasa tangu msanii mwenzangu Steven Kanumba aage dunia, na kama ilivyo kwa kila kitu kinapotokea huandamana na kila aina ya maneno na hisia mbali mbali kutokana na mitazamo ya watu kupishana kuhusiana na jambo husika. Kulingana na muktadha huo, msiba wa Steven Kanumba umekumbwa na maneno na hisia kama hizo, hususan mazingira ya kifo chake; kinachosikitisha zaidi watu wengi (ambao wanajitambulisha kama wapenzi wa Kanumba), na baadhi ya vyombo binafsi vya habari vimekuwa vikinihusisha na kifo hicho, kwa kusema kwamba kwa njia moja au nyingine ninahusika na mauaji ya Steven Kanumba. Kwa muda wote huo tangu msiba ulipotokea mpaka leo hii nashika kalamu kujaribu kuyaweka sawa na kuondosha hisia chafu katika fikra za watu, nimekuwa nikipitia katika wakati mgumu sana kwa jinsi ambavyo nimekuwa nikinyooshewa vidole kila upande nikihusishwa na kifo hicho, kiujumla nimezingatia maoni ya wapenzi ya mashabiki wangu wakinitaka kuwa na subira,  ila kuna ukweli usemao kwamba, uongo ukirudiwa sana jamii huusadiki na kuuona ukweli, nimeona nisikae kimya ila niweke sawa hili kwamba sihusiki na kifo cha Steven Kanumba.
Nasema wazi kwanza sihusiki kabisa na kifo cha Kanumba kwanza kwa kuzingatia mazingira yenyewe ya kifo kilivyotokea. Wakati kifo hicho kinatokea, nilikuwa sehemu nyingine kabisa na mimi nilikuwa mtu wa tatu kutaarifiwa kwamba Kanumba amepatwa na mkasa ambao baadae ulisababisha kifo chake. Na na hata nilipofika katika hospitali ya Muhimbili (tofauti na watu wanavyodhani kuwa nilifika nyumbani kwake; ukweli mimi nilimkuta tayari amepelekwa Muhimbili), nilikuta tayari alikuwa ameshafariki ndio maana hata Polisi wanaohusika na usalama wa raia, si tu kwamba hawakuniweka chini ya ulinzi, sikuitwa hata kuhojiwa kwa sababu hakuna mazingira yoyote yanayonihusisha mimi na kifo hicho.
Pili, watu wanahusisha tofauti za kibinadamu zilizokuwepo baina yetu na kifo hicho, nasema hii sio sahihi kwa sababu kwanza ni kawaida kwa binadamu kutofautiana, isipokuwa kwetu sisi baadhi ya vyombo vya habari vilikuwa vinakuza kwa sababu nisizozijua, hivyo jamii ikachukulia kuwa tofauti zile ni uadui kitu ambacho sio sahihi, kwani sisi hatukuwa watu pekee tunaotofautiana kwani huu ni mwenendo wa kawaida wa dunia; hivi jana tumeshuhudia Waziri mmoja akieleza bayana katika mkutano na waandishi wa habari kuwa na tofauti na naibu wake, lakini hatuajasikia ikiandikwa wana ‘bifu’ bali imetafutwa lugha nzuri ya kupamba tofauti hizo, kwa kuwa waliohusika ni waheshimiwa, ila kwa wengine kutokana na sababu tusizozijua, inaonekana kama ni haki yetu kuandikwa vibaya. Kinachosikitisha, kwa nini jambo hili linachukuliwa kwa mkazo mkubwa sana, kwani hatujawahi kusikia watu wakiwa wanatofautiana na ndugu jamaa hata na marafiki zao na inaonekana kawaida tu? Kwani vyombo vya habari havikuwahi kuandika kuwa marehemu Steven Kanumba alikuwa na tofauti na baba yake, na yeye mwenyewe alitamka hivyo katika vyombo vya habari, mbona wameliongea bila kuongeza chumvi, na jamii inaona kuwa ni jambo la kawaida la kibinadamu.
Pengine watu wanaojaribu kuongea hayo, hawajui mimi na Steven Kanumba tumetoka wapi? Sisi si watu tuliokutana barabarani, tuna historia katika kazi yetu ya sanaa na pia katika maisha maisha yetu. Mwanzoni kabisa, mimi ndiye niliyempokea Kanumba pale Kaole na ndiye niliyemfundisha sanaa pale (nadhani watu wanakumbuka tamthiliya za wakati huo ITV) na baada ya hapo tulienda pamoja katika kampuni ya Game 1st Quality pamoja na tukafanya filamu kama Johari, Sikitiko Langu, Dangerous Disire na nyinginezo, na tuliendelea kuwa pamoja katika kampuni hiyo mpaka tulipofanya filamu ya Oprah mwaka 2008 ambapo niliingia rasmi kufanya kazi za kampuni yangu, lakini tuliendelea kuwa pamoja hata wakati nikiendelea na kazi za kampuni yangu. Pia mimi nilikuwa wa kwanza kuanza kufanya kazi na Steps na baadae Kanumba alipoanza kufanya kazi zake mwenyewe na kunikuta huko tuliendelea kuwa pamoja kama siku zote. Kitu kikubwa kilichokuwa kinaendelea baina yetu, ni kwamba tulijenga ushindani wa kuendeleza kazi mbele kwa kila mmoja akitoa kazi, mwingine anamjibu,  Isitoshe hata vitu vyetu binafsi utaona kama kuna kufanana; kuna wakati Kanumba alinunua Toyota Ruv 4 nyeusi mimi nikanunua ya kijani, aliponunua Harrier na mimi nikanunua pia, na hata gari za hivi karibuni, ukitazama utaona kuwa zinafana kwa karibu; hii ilikuwa ni kama maisha yetu, hatukuwa na uadui, ilikuwa tunapeana changamoto za maendeleo.
 Watu wanaojaribu kuonesha kuwa tofauti zetu ilikuwa ni uadui, huwa hawajui wapi tulikotoka ndio maana wanasema wasemavyo na katika kuthibitisha kuwa tofauti hizo hazikufikia katika uadui, kuna watu ambao wanafanya kazi nami katika kampuni yangu ya RJ ndio hao hao Kanumba alikuwa anawatumia siku zote katika kazi zake, hata baada ya tofauti hizo hakuna aliyekoma kufanya kazi na yeyote kati yetu. Hii inathibitisha kuwa tofauti ilikuwa kati yetu kama binadamu, sio chuki za kimafanikio, ingekuwa hivyo watu kama Junior Syaary ambaye mara nyingi hufanya final editing katika RJ ndio huyo huyo alikuwa akifanya na Kanumba, Ally Yakuti ambaye anaandika script za RJ, ndiye huyo huyo aliyekuwa anaandika kwa Kanumba, Steven Shoo ambaye ni mtaalamu wangu wa light, ndiye huyo huyo anayetumiwa na Kanumba na wengine wengi kama Juma Chikoka aliyecheza kikamilifu katika filamu ya kijiji cha Tambua Haki, ambaye pia anashiriki filamu nyingi za RJ, na wote hao, hawakuanzia kwa Kanumba, wote wameanza kwangu mimi ndio niliompatia na hata baada ya hayo yanayosemwa kuwa kuwa ni uadui, sikuwahi kuwakataza kufanya kazi na Kanumba.
Tatu kumtuhumu mtu kwa namna yoyote ile bila ya uthibitisho wa tuhuma hizo, ni kosa kwa sheria za nchi na pia kama ni mfuasi wa dini yoyote ni dhambi, kwani wakati ukisema hayo huku hujui uhalisia bali unasukumwa na nguvu za hisia tu ni sawa na kumchafua mtu huyo katika jamii bila ya kujua jamii inamchukuliaje. Napenda kusema wazi wazi kuwa, kwa kila anayetekwa na wimbi hili, ajaribu kufikiria leo ipo kwangu mimi, kesho inaweza kuhamia kwako, kwani mimi sio wa kwanza kufikwa na haya, inaweza kukukuta hata wewe au ndugu yako, utajisikiaje. Na kama kweli mimi nimehusika na kifo cha Kanumba kwa namna yoyote ile, basi Mungu atanihukumu na kila aliye hai atashuhudia, ila kama sijahusika kwa lolote, Mungu hatonihukumu na badala yake ataniinua, kwa kuwa ninapita katika kipindi kigumu mno sasa hivi kwa madhila haya.
Mwisho kabisa napenda kumaliza kwa msemo usemao, ajidhaniaye amesimama, aangalie asianguke, kwani kadri mambo haya yanavyoendelea, usidhani yataishia kwangu, kwani mkono wa dhuluma haushii karibu, ukisikia jirani anapiga kelele za mwizi, usilale kamsaidie, usiseme kuwa hatuhusiki kwani hayupo kwetu, kesho utafikwa na wewe utakosa wa kukusaidia. cha msingi kama tunampenda sana ndugu yetu ni kumuombea kwa Mungu, kwani hatujui makao yake huko aliko, na sio kuunda vitu ambavyo kamwe hata yeye angekuwa hai asingeviafiki.
MUNGU AILAZE ROHO YA MAREHEMU STEVEN KANUMBA MAHALI PEMA
 PEPONI
MUNGU IBARIKI AFRIKA MUNGU IBARIKI TANZANIA